Kufuatia kitendo hicho kilichotokea wakati wa mazoezi, TFF imesema tukio lililofanywa na mchezaji huyo ni kinyume na sheria, taratibu/kanuni zinazoendesha mpira wa miguu nchini, hivyo wanakilaani kitendo hicho kwa nguvu zote.
Kwa kuwa tukio lilitokea wakati wa mazoezi, mpaka sasa TFF bado haijapokea taarifa rasmi kuhusiana na suala hilo.
Kiungo huyo Mkongwe anadaiwa kufanya tukio hilo Februari 10 mwaka huu ambapo alifikishwa katika kituo kilicho karibu kabisa na hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa madai ya kumshambulia mwandishi huyo.
Imeelezwa, Kazimoto alimshambulia Mwanahiba baada ya mazoezi ya Simba yaliyofanyika katika uwanja wa Kambarage uliopo katika eneo la Majengo mjini Shinyanga.
Mara baada ya mazoezi, inadaiwa Kazimoto alimvamia Mwanahiba na kumpiga akidai aliandika habari kwamba kiwango chake pamoja na wachezaji wengine katika mechi mbili za Simba dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons hakikuwa kizuri na wanapaswa kuchunguzwa.
Kazimoto alionekana kutofurahishwa na habari hiyo iliyoonekana ni kama tuhuma, hivyo kupandwa na hasira hadi kuingia katika mgogoro huo na Mwanahiba.
Baada ya kipigo hicho, Mwanahiba aliripoti katika kituo hicho cha polisi na kupewa hati ya mashitaka (RB) yenye yenye namba SHY/RB/895/2016, fomu ya matibabu (PF3) kisha akapelekwa hospitali kwa matibabu.
Kazimoto hakupatikana kulizungumzia suala hilo, pia hakuna kiongozi wa Simba aliyelizungumzia, huku kukiwa na hekaheka ya kutaka kulimaliza kwa amani jambo ambalo linaonekana kupingwa na upande wa wanaolalamika.
Kwa upande wake Mwanahiba, alisema aliandika habari iliyokuwa ikieleza viongozi wa Simba kutoridhishwa na baadhi ya wachezaji wa Simba akiwemo Kazimoto baada ya wao kupoteza mchezo kwa kufungwa na Prisons kwa bao 1-0 mjini Mbeya katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara.
Mwanahiba amesema, ilikuwa ni habari ya mwaka jana, na jana Kazimoto akamwita na kuanza kumuuliza akitaka amwambie kiongozi gani aliyemwambia hizo habari za wachezaji na akamjibu sio kazi yake kwani aliyoyaandika aliambiwa na uongozi kama yalivyokuwa.
Mwanahiba amesema, Kazimoto alipoona hoja zinazidi akaanza kumshambulia kwa ngumi na mateke hadi alipomuumiza kichwani na wakati huo wachezaji wengine walikuwa kwenye basi wakishuhudia na ndipo Mussa Hassan Mgosi akawahi kushuka na kumuokoa.





