Ijumaa , 3rd Apr , 2015

Kocha wa Timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars, Rogasian Kaijage amesema, maandalizi kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia The She-Polopolo sio ya kuanza upya bali ni kufanyia marekebisho makosa yaliyopo.

Akizungumza na East Africa Radio, Kaijage amesema, marekebisho hayo ni yale yanayoweza kurekebishika ambayo ni ya muda mfupi kwani kuna marekebisho ya muda mrefu ambayo hayawezi kurekebishika sasa hivi.

Kaijage amesema, wanacholenga hivi sasa ni kurekebisha marekebisho ya muda mfupi ili timu iweze kufanya vizuri na kuweza kupata matokeo mazuri zaidi ya hapo awali.

Kaijage amesema, Kikosi alichonacho hivi sasa kinajijenga kwa Sababu kunamchanganyiko wa wachezaji wapya wengine na hawana uzoefu ambapo kuna mambo ambayo hayawezi kujengwa sasa hivi lakini baadhi ya mambo ya kiufundi yanaweza kurekebishika katika kikosi hicho.

Twiga Stars inatarajia kupambana katika mechi yake ya marudiano na She-Polopolo Ijumaa ya April 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo katika mchezo wa awali uliofanyika wiki mbili zilizopita jijini Lusaka Zambia, Twiga Stars iliibuka na ushindi wa mabao 4-2, mabao yaliyofungwa na Asha Rashid (2), Shelder Boniface (1) na Sophia Mwasikili (1).

Mshindi wa jumla katika mchezo huo atafuzu moja kwa moja kwa fainali za Michezo ya Afrika zitakazofanyika nchini Congo