Jumapili , 3rd Jun , 2018

Wakati tetesi zikieleza kuwa kocha wa Kagera Sugar Mecky Mexime, amefanya mazungumzo na klabu ya Yanga kwaajili ya kuwa kocha, yeye amesema anatarajia kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuifundisha timu yake ya Kagera Sugar.

Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar anatarajia kukutana na mabosi wa Kagera Sugar Jumanne Juni 5, ili kukamilisha mazungumzo na anaamini kila kitu kitakwenda vizuri.

"Wameshanitumia tiketi ya ndege, nitaenda Jumanne kwa ajili ya kwenda kumalizana nao, ila ni kweli Yanga walinifuata na niliitikia wito wao, hii sio mara ya kwanza kuniita lakini hatujawahi kufikia makubaliano," alisema Maxime.

Aidha amesema baada ya kukamilisha mchakato wake, atawakabidhi viongozi mapendekezo ya nyota anaowahitaji kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/19, ambao unatarajiwa kuanza Agosti mwaka huu.

Kagera Sugar imemaliza msimu wa 2017/18 ikiwa katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi baada ya kujikusanyia pointi 37, na imeshinda mechi nane, sare 13 na kupokea kichapo mara tisa.