Jumamosi , 13th Feb , 2016

Timu ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU) imefanikiwa kuingia hatua ya pili ya mashindano ya kombe la Shirikisho Afrika baada ya kupata ushindi wa mezani kufuatia wapinzani wao Timu ya Gaborone United kutoka Botswana kujiondoa katika mashindano.

Afisa habari wa Chama cha Soka Zanzibar ZFA Ali Bakari amesema, amepokea taarifa hiyo kwa njia ya mtandao kutoka Shirikisho la Soka barani Afrika CAF kuwa Gaborone ambao walitakiwa kucheza na JKU Jumapili ya Februari 14 wamejitoa bila ya taarifa yoyote maalum ya kuzingatiwa na CAF.

JKU watamsubiri mshindi kati ya Al Khartoum au SC Villa ambapo timu hizo katika mzunguko wao wa mwanzo wanakutana hapo kesho.

Kwa upande wa mkurugenzi wa idara ya michezo wa JKU Khamis Mohamed amesema wamepokea kwa bashasha na furaha taarifa hizo na kusema kuwa ushindi ni ushindi tu,hata uwe wa mezani

Ameongeza kuwa wao wamejiandaa vizuri na ndiyo maana hawajajitoa, kilichobakia sasa ni maandalizi ya hatua ya pili waliyofuzu.

Mechi ya klabu bingwa barani Afrika kati ya klabu ya Mafunzo ya Zanzibar na AS Vita Club ya Congo DRC itachezwa Zanzibar hii leo saa 10:30 za jioni uwanja wa Amani ambapo kiingilio ni bure.