Jumapili , 12th Feb , 2017

Nahodha wa African Lyon Hassan Isihaka, na mshambuliaji Venance Ludovic, leo wameizuia Mtibwa Sugar kutoka na pointi tatu katika dimba la Taifa Dar es Salaam, kwa kuilazimisha sare ya mabao 2-2

Nahodha wa African Lyon, Hassan Isihaka

Katika mchezo huo wa ligi kuu, Hassan Isihaka ndiye aliyepachika mabao yote mawili kwa African Lyon kwa mikwaju ya penati, ikiwa ni adhabu kutokana na makosa yaliyofanywa na mlinzi wa Mtibwa Henry Joseph Shindika.

Makosa yote mawili yaliyozaa penati yalitengenezwa na Venance Ludovic, ambapo katika kosa la kwanza, Henry Joseph alijikuta akilamika kumkwatua Ludovic ambaye alikuwa amekwisha mtoka na akiwa tayari kumsalimia mlinda mlango wa Mtibwa.

Katika kosa la pili, Ludovic alimnawisha Henry Joseph katika eneo la hatari, na mwamuzi hakuona hiana kutenga mkwaju wa pili wa penati uliofungwa tena na Hassan Isihaka likiwa ni bao la kusawazisha baada ya Mtibwa kuwa wametangulia.

Mabao ya Mtibwa yalifungwa na Jeba, likiwa ni la kusawazisha baada ya African Lyon kutangulia na bao la pili likifungwa na Stamili Mbonde.

Katika michezo mingine, Mwadui imeichapa Mbeya City mabao 3-2 katika dimba la Mwadui Complex Shinyanga, huku JKT Ruvu wakiichapa Mbao FC 2-0 katika dimba la Mkwakwani Jijini Tanga.