Jumanne , 31st Mei , 2016

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amesema kwamba hakuna mchezaji wa kigeni aliyeachwa hadi sasa na kwamba vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti tofauti.

Amesema kwamba walikuwa wakilalamikia uwajibikaji usioridhisha wa wachezaji wa kigeni wa klabu hiyo, lakini hawakusema wanaachwa.

Aidha, Hans Poppe ameongeza kuwa wachezaji wote wenye mikataba na Simba wanaendelea kupewa stahiki zao kama kawaida wakiwemo hao wa kigeni.

Mwishoni mwa msimu, Simba SC ilitofautiana na wachezaji wake wa kigeni baada ya kugoma kwenda Songea kucheza mechi ya pili kuelekea mwishoni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Majimaji.

Wachezaji hao ni kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast, mabeki Emery Nimubona kutoka Burundi, Juuko Murshid, kiungo Brian Majwega, mshambuliaji Hamisi Kiiza wote kutoka Uganda na kiungo Justice Majabvi kutoka Zimbabwe ambao waligoma kwa kucheleweshewa kwa wiki moja mishahara ya Aprili.

Hata hivyo, hivyo Simba SC iliwalipa mishahara yao wachezaji hao na kuteua wawili, Angban na Majabvi kwenda Songea siku moja kabla ya mechi.