Jumanne , 22nd Dec , 2015

Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi kuanzia Desemba mbili mwakani visiwani Zanzibar.

Picha ya nyota wa klabu mbalimbali zilizoshiriki mapinduzi Cup mwaka 2014

Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Kisiwani Zanzibar Kassim Haji Salum amezitaja Klabu za Kenya Gor Mahia na KCCA ya Uganda kuwa miongoni mwa Timu zitakazocheza mashindano hayo.

Klabu kutoka Tanzania Bara ambazo zitashiriki ni Yanga, Simba, Azam FC na Mtibwa Sugar wakati kutoka Zanzibar ni Mafunzo na JKU.

Michuano hii ya Mapinduzi Cup ni muhimu kwa timu za Yanga, Azam FC, JKU na Mafunzo ambazo zitashiriki mashindano ya kimataifa ngazi ya klabu barani Afrika.

Yanga watacheza michuano ya klabu bingwa barani Afrika ikianzia mtoano dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius wakati Azam FC wapo katika Kombe la Shirikisho na watacheza na mshindi kati ya klabu ya Seychelles na Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

Mafunzo wao watacheza na AS Vita ya Congo DR Congo kwenye klabu bingwa barani Afrika na JKU kucheza Kombe la Shirikisho na Gaborone United ya Botswana.