Jumamosi , 26th Jun , 2021

Hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho nchini 'ASFC' itaendelea leo Juni 26, 2021 kwa mchezo mmoja ambapo bingwa mtetezi wa kombe hilo klabu ya Simba inataraji kushuka dimbani saa 9:30 Alasiri kwenye dimba la Majimaji lililopo Songea mjini mkoani Ruvuma.

Kocha wa Simba, Didier Gomez Da Rosa.

Kuelekea kwenye mchezo huo kocha wa Simba, Mfaransa, Didier Gomez Da Rosa amesema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu lakini anaamini kwenye kujituma na kuonyesha uwezo ili kutinga fainali.

“Utakuwa ni mchezo mgumu lakini tunataka kushinda makombe yote la Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho. Tunawaheshimu sababu tunajua vizuri sana uwezo lakini tumejipanga vizuri sana kufika fainali.” 

“Lazima kesho tuonyeshe tunataka kufika fainali kwa kujituma na kuonyesha uwezo. Lazima tushinde Ligi Kuu, lazima tushinde Kombe la Shirikisho, hayo ni malengo yetu.” 

Baada ya  kusema hayo, Nae nahodha wa kikosi hicho John Rafael Bocco amesema wana waheshimu sana wapinzani wao kutokana na ubora walionao lakini anaamini atapata matokeo mazuri.

“Tunaenda kukutana na timu nzuri, tunawaheshimu kwa hilo lakini tumejipanga vizuri na Mungu atatusaidia kupata matokeo mazuri na kufuzu fainali.” 

Kwa upande wa Azam, wamejinasibu kumvua Ubingwa Simba na kuandika historia nyingine kwa kutwaa kombe hilo kwa mara ya pili ndani ya misimu mitatu baada ya mwaka 2019 kuwafunga Lipuli ya mkoani Iringa 2-1 Ilulu mkoani Lindi.

Mara ya mwisho wawili hao kukutana ili tarehe 7 februari mwaka huu kwenye mchezo wa VPL ambapo ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2 lakini tokea septemba 2010, wawili hao tayari wamekutana mara 25, Simba akipata ushindi michezo 9, Azam akishinda michezo 7 na kutoa sare 9.

Mchezo huo pia ni kumbukumbu ya mchezo wa robo fainali ya msimu uliopoita ambapo Simba alifanikiwa kutinga hatua ya fainali na kubeba kombe hilo.