Jumamosi , 29th Mei , 2021

Kocha wa timu ya Geita Gold, Fred Felix Minziro amejinasibu kuibuka na ushindi mbele ya timu ya Mbeya Kwana kwenye mchezo wa fainali ya kutafuta bingwa wa Ligi daraja la kwanza utakaochezwa saa 10:00 jioni ya leo kwenye dimba la Chamazi.

Kocha wa timu ya Geita Gold, Fred Felix Minziro almaaruf 'Baba Izaya'.

Minziro ameyasema hayo muda mchache kuelekea kwenye mchezo husika huku akionekana kujiamini sana na uwezo wa timu yake iliyomaliza kinara wa kundi A ilhali Mbeya Kwanza ilifanikiwa kumaliza kinara w kundi B.

Minziro amesema, “Kesho lazima tucheze kufa na kupona. Wachezaji wapo tayari kupambana. Wapo tayari kufanya maajabu. Hakuna kinachoshindikana. Niwaombe tu mashabiki waweze kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao".

“Tunajua mbeya kwanza ina kikosi bora na ina timu ngumu, lakini hatujali kuhusu hilo, tunajiamini tuna kikosi bora na ni wazi tutaibuka na ushindi kwenye mchezo huo wa fainali ya ligi daraja la kwanza”.

Kwa upande wa kocha msaidizi wa Mbeya Kwanza, Michael Mnyali amesema, “Nilichopenda mchezo wa leo utakua mubashara kwenye luninga ondoeni hofu wapenzi wetu mtashuhudia kabumbu Safi”.

Wawili hao wameshafanikiwa kupanda daraja na watashiriki Ligi kuu ya Vodacom kwa msimu ujao wa mwaka 2021-2022 licha ya kuwa mmoja wapo atapoteza mchezo wa leo ambao lengo lake ni kusaka bingwa mmoja wa Ligi daraja la kwanza.