Alhamisi , 26th Feb , 2015

Chama cha mpira wa Magongo Mkoa wa Dar es salaam kimesema serikali itasaidia kuendeleza programu mpya ya kutoa mafunzo ya mchezo wa mpira wa magongo kwa kukuza na kupata vipaji vipya katika mchezo huo.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa DRHA, Mnonda Magani amesema, wameshapata vibali kutoka serikalini ambapo programi hiyo itashirikisha shule za msingi na Sekondari na baadaye kusambaa katika vyuo vilivyopo jijini Dar es salaam.

Magani amesema, kwa kushirikiana na Chama cha mpira wa magongo Tanzania THA, wanatarajia kutoa mafunzo hayo katika mikoa yote hapa nchini ili kuweza kuwa na vipaji vipya nchi nzima.

Kwa upande wake Mwalimu wa Michezo kutoka Shule ya Sekondari ya Kibasila, Ingridy Kimario amesema wanafunzi wanauwezo wa kufanya vizuri kama wakiwa makini kufundisha watoto.

Kimario amesema, programu hii itachukuwa wanafunzi wa aina mbalimbali ambapo watachukua wale wanaosomea masomo ya michezo na hata wale ambao hawasomei michezo ambao wanapenda michezo.