Jumapili , 11th Mei , 2014

Uongozi wa klabu ya Yanga umesema kuondoka kwa wachezaji wao wawili Didier Kavumbagu na Frank Domayo sio mwisho wa timu hiyo na unaendelea na mipango ya kuhakikisha inasajli wachezaji wengine wazuri zaidi

Baadhi ya Mashabiki wa Yanga wakiwa makao makuu ya klabu hiyo Jangwani Jijini DSM

Uongozi wa klabu ya Yanga umesema kuondoka kwa wachezaji wao wawili Didier Kavumbagu na Frank Domayo sio mwisho wa timu ya Yanga, kwani unaendelea na mipango ya kuhakikisha inasajli wachezaji wengine wazuri ambao wataisadia timu kwenye msimu ujao kwa kufuata maelekezo ya Benchi la Ufundi.

Uongozi wa klabu hiyo umesema kuwa kuondoka kwa Kavumbagu ni kutokana na kuchelewa kwa majibu ya TFF juu ya idadi ya wachezaji wageni kwa msimu mpya, huku Domayo ambae tangu mwaka jana aliombwa kuongeza mkataba alikua akisema anamsubiria mjomba wake ndipo aweze kufanya hivyo.

Umesema kuwa pamoja na kuondoka kwa wachezaji hao bado kwa kushirikiana na kocha Hans watahakikisha Yanga inaendelea kutisha msimu ujao na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.

Hans aliahidi kuleta wachezaji wazuri watakaoisaidia Yanga siku alipokua akiiongea na waandishi wa habari kuwaaga.

Aidha Klabu hiyo imesema kuwa umelifuta rasmi tawi la Tandale kutokana na kuwa ni chanzo cha vurugu na migogoro ndani ya klabu, pia amewafuta uanachama wanachama sita ambao walikiuka katiba ya Yanga kwa kwenda kuongea na waandishi wa HABARI bila ya Idhini ya uongozi huku pia wakishindwa kulipia ada zao za uanachama kwa zaidi ya miezi sita, 

Waliofutwa uanachama ni:
1. Ally Kamtande
2. Isiaka Dude
3. Hamisi Matandula
4. Waziri Jitu Ramadhani
5. Mohamed Kigali Ndimba
6. Selaman Hassan Migali.

Katika hatua nyingine, Klabu hiyo imetangaza tarehe ya mkutano mkuu kwa ajili ya marekebisho ya katiba kuwa utafanyika terehe mosi Juni, 2014 katika Ukumbi wa Oysterbay Police Mess na wanachama wote wanaombwa kulipia ada zao ili waweze kuhudhuria mkutano huo wakiwa hai. 

Kuhusu suala la ujenzi wa Uwanja wa Kisasa eneo la Jangwani klabu hiyo imesema kuwa bado lipo pale pale, kinachosubiriwa ni majibu ya serikali juu ya maombi ya eneo la ziada na kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alisema suala hilo lipo ukingoni na mda si mrefu.