Jumamosi , 23rd Dec , 2017

Mshambuliaji wa klabu ya Azam FC Mbaraka Yusuph, anatarajia kukaa nje ya dimba kwa muda wa wiki mbili baada ya kupata mshtuko mdogo kwenye goti lake la mguu wa kushoto.

Mbaraka amegundulika na tatizo hilo baada ya kufanyiwa uchunguzi kwenye Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo jijini Cape Town, Afrika Kusini chini ya daktari bingwa wa magoti pamoja na nyonga Nickolas.

Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, amesema kuwa mara baada ya mshambuliaji huyo kumaliza matibabu na mapumziko hayo ya wiki mbili ataruhusiwa rasmi kuanza mazoezi madogo madogo.

Yusuph amekwenda nchini humo kwa matibabu sambamba na Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Abdulkareem Amin ambaye ndiye ameshughulikia taratibu zake zote za matibabu.

Nyota huyo alipata majeraha hayo akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ iliyokuwa ikishiriki michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika nchini Kenya wikiendi iliyopita.