
Wakati Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) likimteua Mwenyekiti wa zamani wa baraza hilo, Leodegar Tenga kuwa mwenyekiti wa heshima, limetangaza kuwa mashindano ya mwaka huu ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge yatafanyika nchini Sudan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, mashindano hayo yatafanyika Sudan na tayari Wizara ya Michezo ya nchi hiyo kwa kushirikisha na Chama cha nchi hiyo (SFA) wamethibitisha kuwa wenyeji wa michuano hiyo.
CECAFA pia imeshapitisha kuwa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) mwaka huu yatafanyika Zanzibar wakati ya vijana ya umri chini ya miaka 17 yatachezwa Uganda na Burundi itakuwa mwenyeji wa michuano ya vijana ya umri chini ya miaka 20.
Uganda ndiyo bingwa wa mashindano ya Kombe la Challenge wakati Azam FC ya Tanzania Bara ndiyo wanakishikilia kikombe cha Kagame baada ya kuwafunga Gor Mahia mwaka jana.
Wakati huo huo, mwenyekiti mpya wa CECAFA, Gaffar Mutasin, ambaye ni raia wa Sudan aliahidi kuendeleza soka la wanawake na vijana katika uongozi wake ili kuinua kiwango cha soka cha nchi 12 wanachama wa baraza hilo.