Alhamisi , 22nd Aug , 2019

Bodi ya Ligi (TPBL) imesema haitobadilisha ratiba ya mechi yoyote ya ligi ya msimu huu kama ilivyokuwa misimu kadhaa iliyopita.

Yanga

Kauli hiyo imeelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alipokuwa akijibu kuhusu maombi ya uongozi wa klabu ya Yanga kubadilishiwa ratiba ya mechi yao ya ufunguzi.

Wambura amesema kuwa klabu ya Yanga iliomba kubadilishiwa ratiba ya mchezo wao ambao utachezwa Agosti 28, usogezwe mbele kwakuwa hivi sasa ipo nchini Botswana ambako itacheza mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Township Rollers, Agosti 24, hivyo watakuwa na muda mfupi wa kurejea na kujiandaa na mchezo wa ligi.

"Yanga walituandikia barua kuomba tusogeze mbele mchezo wao, sisi tumewajibu kuwa hatutobadilisha ratiba ya mchezo wowote wa ligi, wao wanasema wanacheza Agosti 24 hvyo wana muda mfupi wa kujiandaa. Lakini sisi ratiba yetu tulishaitoa", amesema Wambura.

Yanga inatarajia kushuka dimbani katika mechi ya ufunguzi wa ligi, Agosti 28 dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa taifa.