Ijumaa , 15th Dec , 2017

Timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) imetinga fainali ya kombe la CECAFA Senior Challenge baada ya kuwaondoa mabingwa watetezi Uganda kwenye mchzo wa nusu fainali uliomalizika jioni hii.

Mchezo huo umepigwa kwenye uwanja wa Moi mjini Kisumu, Zanzibar walifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 22 kupitia kwa Abdulaziz Makame Hassan KABLA YA Uganda kusawazisha dakika ya 28 kupitia kwa Nsibambi Derrick.

Kipindi cha pili Zanzibar walianza kwa kasi wakitumia mbinu za kushambulia kwa kushitukiza ambapo katika dakika ya 58 walifanikiwa kupata Penalti ambayo ilifungwa na mchezaji Mohamed Issa Juma. Bao hilo limeipeleka Zanzibar fainali.

Vijana hao wa kocha Hemed Morocco watakutana na timu wenyeji ambayo ni Harambee Stars. Wenyeji hao walifuzu hatua ya fainali siku ya jana baada ya kuwafunga Burundi kwa bao 1-0 na leo wamemjua mpinzani wao wa fainali.

Kenya na Zanzibar zote zimetoka kundi A ambapo Kenya iliongoza kundi hilo ikifuatiwa na Zanzibara ambayo ilishika nafasi ya pili wakiziacha timu za taifa kadhaa ikiwemo ile ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) ambayo iliondoka na alama moja.