Ijumaa , 28th Aug , 2015

Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania BFT limesema wanaamini uwakilishi wa mabondia waliochaguliwa kuwakilisha nchi katika mashindano ya All Africa Games wataipeperusha vizuri bendera ya nchini Congo Brazzaville.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga amesema mabondia hao wamewachagua kulingana na ubora walipokuwa mazoezini hivyo wanaamini japo nafasi ni chache lakini wanaamini uwakilishi wao utakuwa ni mzuri.

Mashaga amewataja mabondia watakaowakilisha katika michuano hiyo kuwa ni Ismail Galiatano katika uzito wa kilo 60 huku katika uzito wa kilo 56 akiwakilisha Ahmad Furahisha na Uzito wa 52 Said Hofu atawakilisha wakiongozana na Kocha Benjamini Mwangata.

Mabondia hao wanatarajia kuondoka nchini Jumamosi ya Agosti 30 mwaka huu kuelekea nchini Congo Brazzaville kujiandaa na mashindano ya All Africa Games yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba mbili mwaka huu.