Alhamisi , 1st Jan , 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, anatarajiwa kufungua michuano ya Kombe la Mapinduzi inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi leo uwanja wa Aman kwa kuzikutanisha timu ya Azam FC na Mtibwa Sugar.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar ZFA, Khasim Salum amesema katika michuano hiyo, Timu ya Sports Club Villa ya nchini Uganda iliyoalikwa katika michuano hiyo imejitoa kutokana na kuchelewa kufika kwa ajili ya kuanza michuano hiyo.

Salum amesema, SC Villa iliyo kundi A ikiwa pamoja na timu ya Yanga ya Tanzania Bara pamoja na Polisi na Shaba zote za Zanzibar ilitakiwa kukutana na Yanga katika mechi yake iliyotakiwa kuchezwa siku ya Jumamosi lakini kutokana na kujitoa kwa timu hiyo, Yanga itakutana na Timu ya Jang'ombe ya Mjini Magharibi.

Said amesema, fainali za michuano hiyo inatarajiwa kuchezwa Januari 13 usiku katika uwanja wa Aman kwa kuhitimisha michuano hiyo.