Azam FC ilijipatia ushindi huo katika dakika ya tano ya mchezo kupitia kwa mchezaji wake Khamis Mcha ‘Vialli’ aliyepokea pasi ya Michael Bolou na kuwachomoka mabeki wakidhani ameotea.
Azam FC iliweza kufanya mashambulizi kadhaa langoni mwa wapinzani wao, lakini walipoteza nyingi za kufunga mabao na kikwazo kingine kikiwa ni safu ngumu ya ulinzi ya Jang’ombe.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Azam FC iliondoka kifua mbele kwa bao hilo moja, ambapo Kocha Mkuu Zeben Hernandez, aliweza kubadilisha wachezaji nane kilipoanza kipindi cha pili lengo likiwa ni kuwatathimini zaidi wachezaji wake wote.
Walioingia kipindi cha pili ni mabeki Ismail Gambo na Gadiel Michael, viungo Mudathir Yahya, Masoud Abdallah, Salum Abubakar, washambuliaji Brian Abbas, Ibrahima Fofana na Fuadi Ndayisenga, huku waliotoka wakiwa ni David Mwantika, Bruce Kangwa, Himid Mao, Bolou, Mcha, Frank Domayo, Bocco na Ramadhan Singano.
Jang’ombe walionekana kucheza vizuri kipindi cha pili tofauti na kipindi cha kwanza, jambo lililowapa wakati mgumu Azam FC licha ya kufanya mabadiliko.
Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa Azam FC katika kambi ya Zanzibar baada ya ule wa kwanza uliofanyika Jumatano iliyopita Azam FC kuibuka kwa ushindi mwingine wa bao 1-0, lililofungwa na Fuadi Ndayisenga aliyeko katika majaribio.
Mara baada ya Azam FC kumaliza ziara yake hiyo, leo kikosi kimewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na programu yake ya maandalizi ya msimu ujao.
Kikosi Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Bruce Kangwa/Gadiel Michael dk 46, David Mwantika/Ismail Gambo dk 46, Aggrey Morris, Jean Mugiraneza, Himid Mao/Masoud Abdallah dk 46, Michael Bolou/Mudathir Yahya dk 46, Frank Domayo/Salum Abubakar dk 46, Khamis Mcha/Fuadi Ndayisenga dk 46, John Bocco (C)/Ibrahima Fofana dk 46, Ramadhan Singano/Brian Abbas dk 46.






