Alhamisi , 31st Jul , 2014

Kocha mkuu wa timu ya soka ya Azam FC mcameroon Joseph Omog amesema njia pekee ya kuwapa uzoefu na kugundua mapungufu ya kikosi chake ni kucheza michezo mingi ya kujipima uwezo na timu ambazo zina ushindani wa kutosha

Kikosi cha mabingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL 2014-2015 Azam FC.

Mabingwa wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Azam FC ya jijini Dar es salaam imendelea na mazoezi ya maandalizi ya ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL na michuano ya klabu bingwa barani Afrika

Afisa habari wa timu hiyo Jafari Idd Maganga ‘mbunifu’ amesema mipango ya mwalimu Mcameroon Joseph Omog ni kuona timu hiyo inakuwa imara na bora zaidi ya msimu uliopita ambao walifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu

Jafar amesema wamekuwa wakifanya mazoezi kwa takriban majuma manne sasa na kocha mkuu wa timu hiyo amependekeza kila juma wacheze mechi mbili za kirafiki katika siku za Jumanne na Alhamis ili kufanya marekebisho yaliyopo.

Aidha Jafar amesema wameshacheza michezo ya kirafiki na timu za JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Police Morogoro na Friends Rangers na kwa sasa bado wanachangamoto kubwa ya kupata timu zaidi za kucheza nazo kwakuwa ligi imesogezwa mbele hadi September 20 timu nyingi zimesimamisha mazoezi na hivyo inawapa wakati mgumu wa kupata timu za kucheza nazo na hivyo kulazimika kurudiana na timu walizocheza nazo awali ambazo nazo zinaendelea na mazoezi.