Akizungumza jijini Dar es salaam wakati ya uzinduzi wa mashindano ya soka kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars, Mkurugenzi wa idara ya michezo, vijana, utamaduni na michezo, Leonard Thadeo amesema, michuano hiyo inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi katika hatua za awali Agosti nane itashirikisha timu za wavulana na wasichana katika mikoa mbalimbali ni fursa pekee kwa vijana wakike kuonesha vipaji walivyo navyo na pia ni jukwaa muhimu kwa makocha wa timu za wanawake kuweza kubaini wachezaji wenye vipaji kwa ajili ya timu mbalimbali za wanawake.
Thadeo amesema, jamii inatakiwa kuziunga mkono timu za wanawake ili kuweza kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali ikiwemo yale ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Septemba mwaka huu nchini Congo Brazzaville ambapo timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars imejihakikishia kushiriki mashindano hayo.
Mashindano hayo kwa mwaka huu ambao ni msimu wa tano yatajumuisha mikoa ya Ilala, Kinondoni, Temeke, Mbeya, Mwanza na Morogoro kwa upande wa wavulana huku kwa upande wa wasichana ukiwakilisha na mikoa ya Ilala, Kinondoni, Temeke, Mbeya na Arusha ambapo yatahitimishwa kwa fainali za Taifa jijini Dar es salaam Septemba 11 mpaka 21 mwaka huu.

