Jumatano , 4th Feb , 2015

Klabu ya Simba imesema haijamfukuza mchezaji wake Shaban Kisiga isipokuwa mchezaji huyo aliondoka bila kutoa taarifa baada ya mechi dhidi ya Mbeya City ambapo mpaka sasa wamemtafuta bila mafanikio.

Akizungumza na East Africa Radio, Msemaji wa Timu hiyo, Humphrey Nyasio amesema, mpaka sasa uongozi wa juu unashughulikia suala la Kisiga ambaye hajawasili kambini wiki mbili sasa na walitarajia awe kambini na wachezaji wenzake ili kuendelea na mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya mechi mbalimbali za ligi kuu Tanzania Bara.

Kwa upande mwingine, Nyasio amesema wanaendelea na maandalizi ya Mechi dhidi ya Coastal Union ambapo timu imeondoka leo kuelekea jijini Tanga kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi uwanja wa Mkwakwani.

Nyasio amesema, katika mchezo huo watamkosa mchezaji Said Ndemla ambaye yupo katika mapumziko ya wiki mbili ili kuweza kupona kabisa huku wachezaji Joseph Owino na Hussein Shariff Cassilas wakiendelea na mazoezi.