Alhamisi , 10th Dec , 2015

Shirikisho la masumbwi nchini PST limempongeza Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kwa kuteuliwa kuwa waziri mpya wa wizara ya utamaduni, wasanii na michezo.

Katibu wa zamani wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ambaye kwa sasa ni Waziri wa wizara ya utamaduni sanaa na michezo akizungumza na waandishi wa habari kipindi cha nyuma.

Shirikisho la masumbwi nchini PST limempongeza Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye kwa kuteuliwa kuwa waziri mpya wa wizara ya utamaduni, wasanii na michezo.

Akizungumza na East Africa Radio Katibu mkuu wa PST Anthony Lutha amesema ana imani kuteuliwa kwa kiongozi huyo kutaleta mabadiliko kwenye sekta ya michezo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikifanya vibaya kutokana na uwezo wa baadhi ya viongozi aliowaita wababishaji.

Lutha amemtaka waziri huyo kuhamishia nguvu zake zote kwenye idara hiyo kama alivyofanya akiwa kama katibu mwenezi wa chama cha mapinduzi kwa kuthubutu kuwakemea mawaziri walioonekana mizigo ndani ya chama hicho.

Mapema hii leo akitangaza Baraza la Mawaziri leo Ikulu mjini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Joseph Magufuli amesema Nnauye ndiye waziri wa wizara hiyo ambayo anahitaji nguvu ya ziada kuhakikisha inaboreshwa na kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya michezo nchini.

Awali, wizara hiyo ilikuwa inajulikana kama Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini Dkt Fenella Mukangara, ambaye Naibu wake alikuwa Amos Makala na baadaye Juma Nkamia.