Jumatatu , 20th Jun , 2022

Rais wa Rotary Kimataifa, Shekhar Mehta leo Juni 20 alitembelea vyombo vya habari vya IPP, ambapo akiwa East Africa TV na East Africa Radio alikabidhi taulo za kike pakiti 10500 zilizotolewa na taasisi yake kwa ajili ya kampeni ya Namthamini.

Rais wa Rotary Kimataifa, Shekhar Mehta (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa IPP, Bw. Abdiel Mengi (kulia) ndani ya ofisi za East Africa TV na East Africa Radio.

Msaada huo wa Rotary utakwenda kusaidia wanafunzi wa kike zaidi ya 800 mashuleni kwa mwaka mzima.

Mwenyekiti wa IPP, Abdiel Mengi amezungumza katika tukio hilo kwa kusema, toka kuanzishwa kwa vyombo vya habari vya IPP waasisi wake walifanya masuala mbalimbali ya kuhudumia jamii, na mpaka sasa kupitia kampeni ya Namthamini imeshawafikia wanafunzi wengi katika mikoa mbalimbali Tanzania.

Rais wa Rotary Oysterbay, Aisha Sykes naye alizungumza kwa niaba ya Rais wa Rotary Kimataifa, kwa kusema tangu waanzishe elimu ya masuala ya hedhi, wameweza kuwajengea uwezo wanafunzi kupitia kampeni ya Namthamini na kuwainua mabinti wanaotoka kaya masikini na kusisitiza wataendelea kuchangia kampeni hiyo.

Pia Rais wa Rotary Kimataifa, Shekhar Mehta siku ya leo alitembelea miradi mbalimbali inayofanywa na taasisi yake katika shule ya sekondari Mtakuja maeneo ya Kunduchi, Dar es Salaam ambayo inagusa hedhi salama na kuinua kiwango cha elimu nchini.