Jumapili , 1st Jan , 2023

Muandaaji wa kipindi cha MamaMia cha East Africa Radio, Anna Abdallah Sombida amefanikiwa kushinda tuzo ya 'Best Radio Producer' kwenye hafla ya utolewaji wa tuzo za uandishi wa habari za watoto zilizotolewa na Jukwaa la Wahariri (TEF) kwa kushirikiana na UNICEF Tanzania.

Muandaaji wa kipindi cha MamaMia cha East Africa Radio, Anna Abdallah Sombida akipokea cheti baada ya kushinda tuzo.

Anna Sombida amesema, tuzo hiyo imempa nguvu na motisha ya kufanya kazi kwa bidii zaidi, kwani kitendo cha kupata tuzo hiyo kimemuonesha kuwa kumbe kazi anayoifanya inaonekana na ina nguvu kubwa, huku akiwashukuru TEF na UNICEF Tanzania kwa kutambua mchango wa waandishi wa habari katika jamii.

Anna Sombida amesema kuwa, East Africa Radio ina mchango mkubwa sana katika kumkuza na kumfikisha hapo alipo, kwani amekuwa akipewa nafasi ya kujifunza vitu vingi na kuongozwa vizuri kitu kilichopelekea kukomaa zaidi katika nafasi yake hiyo ya uandaaji wa vipindi.

Pia amewataka waandishi wengine wa habari kutokukata tamaa na kuchangamkia fursa pale zinapotokea, na ikitokea hawajafanikisha wasikate tamaa kwani hata yeye hii si mara ya kwanza kushiriki katika tuzo hizo, mwaka jana alishiriki lakini hakufanikiwa kupata lakini amekuja kupata mwaka huu.