Jumanne , 5th Jul , 2022

Staa wa bongo fleva, Mwasiti Almasi leo alifika katika ofisi za East Africa TV na East Africa Radio na kukabidhi mchango wa taulo za kike pakiti 72 kupitia kampeni ya Namthamini ambazo zitakwenda kusaidia wanafunzi 7 shuleni kwa mwaka mzima.

Mwasiti akiongea kwenye kipindi cha Mama Mia cha East Africa Radio siku ya leo.

Mwasiti ni miongoni mwa wasanii waliokuwepo katika uzinduzi wa kampeni ya Namthamini iliyofanyika Mei 27 mwaka huu katika shule ya sekondari Kidete, Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam.

Hedhi imekua kikwazo kikubwa sana katika elimu ya mtoto wa kike, kwani wapo wanaoshindwa kwenda shule siku 3 hadi 7 kwa sababu ya maumivu makali wakati wa hedhi, na wengine kwa sababu ya ukosefu wa taulo za kike za kujihifadhi hivyo anaweza kubaki nyumbani hadi amalize hedhi.

Mwasiti anasema anatambua changamoto wanazokumbana nazo wanafunzi wa kike shuleni wakikosa taulo za kike za kujihifadhi katika kipindi cha hedhi, moja wapo ni kushindwa kufika shule.

Kampeni ya Namthamini imelenga kuwasaidia wanafunzi wanaotoka katika familia duni nchini kwa kuwapatia taulo za kike na kuhakikisha hawakosi tena masomo pindi wanapokuwa katika siku zao za hedhi na kuwaongezea uwezo wa kujiamini, kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto zao.

Mwasiti ametoa wito kwa wasanii wa kike nchini kama Linah, Nandy, Dayna Nyange, Maua Sama, Haitham, Saraphina na Zuchu wajitokeze kuwasaidia wanafunzi wa kike waweze kupata mahitaji muhimu shuleni.