Ibrahim Ajibu - Mshambuliaji wa Simba
Bao hilo lilikataliwa na waamuzi kwa madai kuwa Ajibu alikuwa ameotea kabla ya kufungwa.
Akizungumza na mashabiki wa soka nchini kupitia kipindi cha KIKAANGONI kinachoruka LIVE kupitia ukurasa wa Facebook wa EATV, Msuva amesema kwa mtazamo hakuona tatizo lolote kwa bao lile, na kwamba alishangazwa na maamuzi ya mwamuzi kudai kuwa Ajibu alikuwa ameotea.
"Wakati bao likifungwa mimi nilikuwa bado sijaingia, nilikuwa benchi, kwaiyo kwa pale uwanjani ni ngumu sana kuwa na uhakika kama aliotea au alikuwa hajaotea, lakini tulipokuja kuangalia marudio kwenye video niliona vizuri, wakati pasi ile inapigwa kwa Ajibu alikuwa hajaotea na alifunga bao zuri ambalo kwa mtazamo wangu ni bao halali, lakini kwa kuwa waamuzi wanaona vizuri zaidi yangu, walikuwa sahihi pia kulikataa kwa kuwa wao ndiyo wenye maamuzi". Alisema Msuva.
Simon Msuva akiwa Kikaangoni, EATV
Akizungumzia bao lililofungwa na Tambwe katika mchezo ule, Msuva amesema pia lilikuwa ni bao halali kwa kuwa mpira ndiyo ulifuata mkono wa Tambwe kabla hajafunga, na kwa kuwa mwamuzi aliamua liwe bao, kwake yeye ni bao halilali.
Kuhusu bao la la kusawazisha ambalo Simba walilipata kupitia kwa Shiza Kichuya dakika za mwisho, Msuva alisema bao lile liliwaumiza kabisa na kuwatoa kwenye mchezo kwa kuwa ni jambo ambalo hawakutegemea na kwamba hadi dakika ile ya 87 walikuwa wanajua kuwa tayari wameondoka na ushindi licha ya kukiri kuwa Simba walibadilika dakika za mwisho na kuongeza ushindani.
Alisema yeye na wachezaji wenzake Yanga wamejipanga vizuri na watahakikisha wanapata ushindi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Simba utakaopigwa Februari mwakani huku akisisitiza kuwa Yanga ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu Bara kwa mara ya 3 mfululizo.