Alhamisi , 26th Nov , 2015

Msanii 20 Percent amesema iwapo wasanii watakuwa na umoja thabiti wenye nguvu, wanaweza kudhibiti wizi wa kazi zao na kuongeza kipato kwao.

20% ameyasema hayo alipokuwa akiongea na timu ya Planet Bongo ya East Africa Radio, na kusema kwamba kuiachia serikali pekee na vyombo vinavyowasimamia si suluhisho pekee la kudhibiti wizi huo.

“Cha kwanza kinatakiwa kitoke kwetu sisi wenyewe, kile kinachoitwa umoja kisiimbwe tu, umoja unatakiwa uonekane, jukumu la kwanza la COSOTA kwa sababu wanamuziki hawana uwezo wa kuanzisha chama chao wenyewe wanamuziki na kukienzi na kudhani kwamba ndio kimbilio lao, kwa hiyo lazima tujue sisi umoja wetu unajengwa na baada ya hapo tutaweza kusonga mbele”, alisema 20 %.

Mwanzoni mwa wiki hii wasanii walikuwa na semina iliyokuwa ikiendeshwa na COSOTA kujadili mustakabali wa kazi zao, hususan suala la mirabaha na hakimiliki.