Sipaswi kuonekana hivi- Beka Flavour

Thursday , 7th Dec , 2017

Msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye awali alikuwa kwenye kundi la Yamoto Band na sasa anafanya muziki mwenyewe, Beka Flavour, amesema kwa alipofikia yeye hapaswi kuonekana chipukizi kwani alishakuwepo kwenye game kitambo.

Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Beka amesema kitendo cha kutoka kwenye kundi na kuanza kufanya muziki mwenyewe hakumfanyi kuwa chipukizi, kwani tayari ana kazi bora mtaani na alishajulikana  kwa siku nyingi.

"Kwa upande wangu mimi nahisi sipaswi kuonekana up coming, mi sijaanza kuonekana leo nimeonekana kitambo japo nilikuwa na Yamoto kule nilikuwa nafanya muziki na huku nafanya muziki pia, ila kilichotofautiana ni kule nilikuwa nafanya kwenye band huku nafanya kama solo artist", amesema Beka Flavour.

Mpaka sasa Beka ameshaachia kazi 5 tangu atoke kwenye Yamoto Band, kazi ambazo tatu aliziachia rasmi kwenye media na mbili aliziachia kimya kimya.