Alhamisi , 7th Jan , 2016

Msanii Q Chief ametangaza kujitoa kwenye uongozi wake unaomsimamia wa QS J Mhonda, kwa madai kuwa kuna mambo yaliyokiukwa kwenye mkataba.

Q chief ameyasema hayo alipokuwa akiongea na mwandishi wa East Africa Radio/EATV, na kusema kuwa ingawa QS J Mhonda amemfikisha hapa alipo sasa, ameona ni vema afanye hivyo ili kutetea haki yake kwa faida ya watoto wake.

“Kuna mis-understanding ambayo inaendelea kati yangu na QS J Mhonda, ni mis-understanding kuhusu mkataba ambao tunasign mi ne yeye, na kwamba kuna vipengele ambavyo inabidi viangaliwe vifanyiwe kazi, unajua mkataba wako ndio maisha yako kwa hiyo mimi nilichofanya ni kumwambia with all respect naheshimu wapi umenitoa, wapi unakusudia kunipeleka lakini tukae chini kuangalia huu mkataba kwa sababu yangu na watoto” alisema Q Chief.

Q chief amesema pamoja na hayo kuna watu wengine kwenye kampuni hawatambui mchango wake, hivyo ameona ni bora akae pembeni mpaka pale watakapomaliza tofauti zao, kwani pamoja na kujitoa huko ni mtu ambaye anamuheshimu na kumkubali.

“Siwezi kusema nimejitoa kwa kumkashifu hapana, ni mtu ambaye namkubali sema kuna makosa machache, kuna watu ambao wameongezeka ambao hawajui kwamba watu wanapigania kampuni, hawathamini kile ambacho we unachofanya au hawakioni, mi nimeona hii sio sawa kwa hiyo narudi pale pale, nataka tu kujihakikishia maisha mazuri”, alisema Q Chief.

Pia Q Chief amesema amempa muda na bado ataendelea kumpa muda kwa sababu ni mtu ambaye ameacha mambo yake yote kwa sababu yake, lakini kusiwe na kona kona, na kwamba amefanya makosa mengi sana huko nyuma, hivyo hataki kufanya tena hayo makosa.