Jumamosi , 17th Feb , 2018

Mwenyekiti wa serikali za mtaa wa Mbweni Teta, Abdallah Mrisho amefunguka na kudai sio kweli nyumba ya msanii Fid Q imejengwa katika kiwanja kisicho rasmi kwa shughuli za makazi bali watu wanafananisha na eneo hilo na nyumba ya serikali za mtaa huo.

Mrisho ametoa ufafanuzi huo wakati alipokuwa anazungumza na eNewz kutoka EATV baada ya kuibuka tetesi kuwa Fid Q ameingizwa 'mkenge' kwa kuuziwa kiwanja kisicho rasmi katika shughuli za makazi na kulazimika nyumba hiyo aliyojenga kuvunjwa ili kupisha shughuli za serikali ziweze kufanywa.

"Kwa ufahamisho tu zaidi katika upande wa 'block 4' nyumba ya kwanza kabisa ni ya Fid Q na ya mwisho kabisa katika mtaa huu naishi mimi mwenyewe. Labda niwatoe wasiwasi kwa wale waliokuwa wanasikia kwamba Fid Q amejenga nyumba katika eneo la wazi na nyumba kuwa ipo hatari kuvunjwa niseme tu hapana labda hawakuweza kupambanua kati ya nyumba yake na nyumba ya ofisi za serikali za mtaa kwa sababu hivi vitu vinashabiana", amesema Mrisho.

Kwa upande wake, Fid Q alipofuatwa kuzungumzia suala hilo hakuweza kusema lolote zaidi ya kusema anashukuru.

Mtazame hapa chini Fid Q akishikwa na kigugumizi kuzungumzia suala hilo.