Jumatatu , 9th Jan , 2017

Katika kile kinachoonekana kuwa ni muziki wa taarab kuongeza mapambano dhidi ya muziki wa bongo fleva, Bendi ya Taarab ya Wakali Wao imetangaza rasmi kupunguza urefu wa nyimbo zao kuanzia sasa.

Thabit Abdul (Kushoto) akiwa na Khadija Yusuph ndani ya FNL

Akizungumza katika kipindi cha FNL cha EATV, mkurugenzi wa bendi hiyo, Thabit Abdul amekiri kuwa ni kweli muziki wa bongo fleva umeifunika kabisa taarab, na kwamba sababu mojawapo ni malalamiko kutoka kwa wadau kuhusu urefu wa nyimbo za taarab.

Thabit ambaye alikuwa akimtambulisha rasmi Khadija Yusuph kama muimbaji mpya kwenye bendi hiyo, amesema mkakati mwingine walionao ni wa kutoa nyimbo nzuri na zenye ushindani zinazoweza kuwaacha watu na maswali huku zikiwa na ujumbe wenye uhalisia katika maisha, jambo ambalo tayari wameshalifanya katika albam yao mpya.

"Ni kweli taarab imefunikwa, lakini sasa tunakuja na mikakati mipya ya kuirudisha taarab, kuusu malalamiko ya urefu nyimbo zetu ambazo zilikuwa zinafika hadi dakika 30 kwa wimbo mmoja, tumelifanyia kazi kwenye nyimbo zetu mpya na sasa hakuna wimbo mrefu kama zamani, zote ni fupi" Alisema Thabit

Thabit amewataka wapenzi wa muziki huo kuitafuta albam mpya ya Wakali Wao yenye nyimbo kama vile Yataka moyo, sina uzuri wa sifa, wapambe macho kodo na nyingine nyingi.