Nimechagua kuwa huru - Nay wa Mitego

Wednesday , 11th Oct , 2017

Msanii Nay wa Mitego amewataka mashabiki wake wamuache apumue kwa kumsakama kwamba kafulia, huku akisema maisha anayoishi sasa ameyachagua na anakuwa huru zaidi.

Akiongea na mwandishi wa East Africa Television, Nay amesema maisha ya kutembea kwa miguuu au kupanda bajaji ni maisha yake aliyokulia, kwani hata marafiki zake ni watu wa kawaida, na pia hapendi kuishi maisha ya umaarufu kama ambavyo wasanii wengi wanafanya.

"Jamai niacheni nipumue, haya ndio maisha yangu niliyoyachagua, kupanda bajaji au daladala ni sehemu ya maisha yangu, mimi nimetokea mtaani siwezi kuishi bila kuheshimu mtaa, hata marafiki zangu ukiwaangalia ni wa kawaida sana, kwa hiyo kutembea kwa miguu isiwe sababu, halafu kama hujagundua mimi napenda maisha ya kawaida, siishi kistaa kama wengine, na pia nikiishi hivi nakuwa huru zaidi", amesema Nay wa Mitego.

Hivi karibuni msanii huyo amekuwa akiandamwa na badhi ya watu kwa kuuza magari yake na kuonekana akitembea kwa bajaji au miguu sehemu mbali mbali.