Jumamosi , 1st Sep , 2018

Mkuu mpya wa Bendi ya Vijana Jazz CCM, James Rock Mwakibinga, amesema atahakikisha bendi hiyo inafufuka na kuandaa nyimbo nzuri zitakazotumika katika chaguzi zote kuanzia zile za serikali za mitaa mwakani na uchaguzi mkuu 2020.

Wasanii Mzee Chilo kushoto, Mwana FA na Mwasiti.

Mwakibinga ameyasema hayo baada ya jana kuteuliwa kuwa msimamizi mkuu wa bendi hiyo, huku akipewa jukumu la kuhakikisha wanaandaa nyimbo nzuri ambazo zitatumika ili chama hicho kiondokane na utegemezi wa wasanii.

''Nafasi hii ni kubwa lakini nitajitahidi kuitendea haki na kujenga bendi iliyo imara kwaajili ya kutoa taswira ya chama chetu na ninaamini tutakuwa na nyimbo zetu nzuri kama vijana wa UVCCM ambazo chama kitazitumia kwenye kampeni'', amesema.

Mkuu mpya wa Bendi ya Vijana Jazz CCM, James Rock Mwakibinga.

Katibu mkuu wa CCM Taifa Dkt. Bashiru Ally, alimtangaza Mwakabinga kama mkuu mpya wa bendi ya Vijana Jazz ndani ya CCM huku akitoa maelekezo kuwa ni lazima bendi hiyo ibebe hamasa ya taifa kwa nyimbo zenye uzalendo kwa taifa na chama.

Pia Dkt. Bashiru Ally alitumia nafasi hiyo kuweka wazi kuwa katika kampeni za uchaguzi ujao hawatahitaji kutumia nyimbo za wasanii wa Bongofleva kwani watakuwa na bendi yao ambayo itasimamia suala la burudani.