Ijumaa , 19th Jul , 2019

Mwanamuziki maarufu nchini Marekani, Beyonce ameendelea kusakamwa na raia wa Afrika Mashariki kutokana na kitendo cha kutumia misamiati ya lugha ya Kiswahili katika filamu yake ya 'The Lion King' bila kutoa shukrani au thamani kutoka kwenye asili ya maneno hayo.

Beyonce na Salim Kikeke

Mtangazji na mwanahabari maarufu kutoka kituo cha BBC Swahili, Salim Kikeke amemtumia ujumbe staa huyo wa RnB na Pop duniani akisema kuwa hajaridhishwa na kitendo chake cha kutowashukuru Watanzania na wana Afrika Mashariki kwa kutumia baadhi ya maneno katika Kiswahili.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Instagram, Kikeke ameandika, “mpendwa Beyonce, Mimi ni mpenzi mkubwa wa kazi zako, Nimeona wasanii uliowachagua kwenye Album yako mpya ya The Gift, Nimefadhaika kutoona hata msanii mmoja kutoka Africa Mashariki hasa Tanzania, Filamu yako ya The Lion King imesetiwa na fahari ya bara la Africa kama Serengeti ambayo ipo Tanzania, neno la hakuna matata na Simba ni maneno ya Kiswahili ambayo yanatumika Tanzania na Africa Mashariki.”

"Kuna baadhi ya maneno ya Kiswahili ametumia kwenye wimbo wake wa Spirit, na hawezi kupata maana halisi Kiswahili kwa kuweka wasanii ambao wanatokea Afrika Magharibi peke yake, haijalishi wana uzuri kiasi gani, hata Tanzania na Afrika Mashariki kuna wasanii wenye vipaji ambao wangekuwepo kwenye hiyo kazi yako mpya”, ameandika Salim Kikeke.

Mapema wiki hii msanii Beyonce alizindua filamu yake ya The Lion King, Pia akataja wasanii wa bara la Africa ambao watakuwepo kwenye Album yake mpya ya 'The Gift'. na wasanii hao wote wanatokea katika nchi za Afrika Magharibi.