Afisa Habari wa BASATA Bw. Aristides Kwizela (wa kwanza kulia) akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa East Africa Television, Bw. Roy Mbowe na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa Vodacom Tanzania, Bi. Nandi Mwinyombella.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza hilo Afisa Habari wa BASATA Bw. Aristides Kwizela, amesema kitendo hicho ni kitu kizuri kwani kinaonesha kuthamini mchango wa kazi za sanaa, pamoja na wasanii wenyewe.
"Kwa niaba ya BASATA na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania, nianze kwa kuwapongeza sana East Africa Television kwa sababu ni kituo cha kwanza ambacho kimeona kuna haja ya kuja na tuzo ambazo kwa kweli ni kuthamini mchango wa wasanii, ambazo wamekuwa wakijitolea kufanya kazi ngumu, wanabuni kazi ambazo zina ubora kwa kweli, na wao wameona kama kituo cha radio na TV ambacho kinatumia maudhui makubwa ya kazi za wasanii, wameona ni vema wakaja na tuzo hizi", alisema Bw. Kwizela.
Pamoja na hayo BASATA wamewataka wasanii kufanya kazi zenye ubora zaidi, ili ziweze kuwa na viwango vizuri kwenye ushindani wa tuzo hizo, pamoja na soko la kimataifa.
"Niwaombe wasanii sasa wafanye na kubuni kazi zenye ubora zaidi, ili ziweze kuingia kwenye hizi tuzo, lakini pia zinazozingatia maadili na utamaduni wa Mtanzania, katika kuleta maudhui yake kwa jamii, na pia ili ziweze kuwa na ushindani kwenye soko la kimataifa", alisema afisa habari wa BASATA, Bw. Aristides Kwizela.