Alhamisi , 26th Nov , 2015

Msanii Peter Msechu amesema kwa sasa hawezi kufanya kazi na msanii mwenzake Baba Levo toka Kigoma, ambao walikuwa marafiki wakubwa kwa kuwa sasa ameshaingia kwenye siasa.

Peter Msechu ameyasema hayo kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, na kusema kwamba kitendo cha baba Levo kuingia kwenye siasa amepotea njia.

“Siwezi kufanya kazi na diwani ambaye ameamua kuacha muziki na kufuata siasa, pesa ya muziki imemshinda Baba Levo, baba levo muziki umemtoa knock out, amekosa hela amekimbilia kwenye hela za serikali, sasa mi ninachopenda kumuarifu baba Levo umeula wa chuya, ntakapokuja kufanya show Kigoma naomba uniandalie mazingira mazuri ya hoteli na uhakikishe napata ulinzi wa kutosha”, alisema Peter Msechu.

Peter Msechu ameendela kwa kusema kwamba anajua kwa sasa atapitia wakati mgumu wa kupata vibali atakapoenda Kigoma, na kwamba Baba Levo u star umemshinda na atahakikisha hafanikiwi.

“Mimi Msechu ndo star kuliko wewe Baba Levo, ingawa napata wakati mgumu sana kwa sababu nikiomba kibali cha show Kigoma, ukiwa kama diwani utanisulubu sana, lakini ntakunyoosha, naamini hautofika popote, huu ni mwaka wako tu watakufukuza kwenye huo udiwani ndani ya siku mbili, utarudi huku muziki ushabadilika na ntakunyoosha, kwa hiyo sasa hivi ninyooshe tu wewe ni mtumishi wa umma nakutakia kila la heri”, alisema Msechu.