Picha ya msanii Professor Jay, Jay Moe na Izzo Bizness
Miaka kama 10 iliyopita mwanamuziki nguli wa Hip Hop nchini Professor Jay aliachia wimbo unaitwa “Tathimini” ambao unapatikana kwenye album yake ‘Machozi, Jasho na Damu’ alimshirikisha Rapper Jay Moe na kikubwa walizungumzia mambo mengi humo ndani, ikiwa ni pamoja na mtazamo wao juu ya muziki wa Rap jinsi ulivyo asisiwa, changamoto mpaka mafanikio yake.
Wimbo huu ulilenga kuwafungua watu akili na kuielewa kazi ya muziki/sanaa na kuwaondoa ile dhana potofu iliyokuwa imejengeka miongoni mwao kuwa ni uhuni, na kutoa mtazamo wao kwa wasanii wengine wa Hip Hop kuwa Rap ni wito, yataka utashi na ufahamu, elimu ya mtaani, kujituma na pia nidhamu, huku pia kuna lines za kuonya wale wanaokiuka misingi ya muziki huo ili tu waheshimiwe, “na mnaovunja miiko ya rap jihukumuni”.
Ukirudi kwenye wimbo wa Rapper Izzo Bizness “Game ya Bongo” aliomshirikisha Jay Moe na One Six unaopatikana kwenye Extended Play (EP) ya ‘The Capricorn’ unasimulia ukweli na mwenendo wa tasnia ya muziki nchini Tanzania jinsi inavyochosha kutokana na kujaa ukiritimba ambao unauwa tasnia ya sanaa.
Ukiritimba huo umesababisha wasanii wenye vipaji wasipewe thamani, baadhi ya wasanii kuacha muziki, kupakaziwa mambo ya hovyo, muziki mbaya kupewa nafasi, wasanii wakongwe kuwa mafukara, wadau kujaa vinyongo nakadhalika.


