
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe kushoto, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe kulia
Machange amesema kwamba Muswada huo utasaidia kuondo U-mungu mtu kwenye vyama vya siasa kwani wapo viongozi ambao wakiwa madarakani wanataka waongoze mpaka kifo.
"Nimekuwa mwanachama mwandamizi wa CHADEMA, ACT Wazalendo, ninaposema umungu-mtu najua maana yake. Zitto Kabwe, Mbowe na maalim Seif wao hawataki, wanachotaka ni ukiwa kiongozi, uongoze hadi kifo, mimi na wanasiasa wengine wadogo tuliowahi kukandamizwa na kuonewa na viongozi wa vyama tunaunga mkono mswada huu", amesema Machange.
Hata hivyo ameshangazwa na suala la kina Zitto kufungua kesi kwa ajili ya mabadiliko ya sheria, akisema kuwa hakuna muujiza unaoweza kupatikana mahakamani.
"Kufungua kesi ni haki ya kikatiba na kisheria, sawa, lakini unafungua kesi kushtaki nini?, wanashitaki eti mswada utavunja haki zao, sijawahi kushuhudia mahakama kuhukumu jambo kwa hisia, nataka mjue kuwa hakuna muujiza utakofanywa na hiyo 'petition' yao mahakamani", Machange.
Amekanusha kuwa si kweli muswada unampa nguvu msajili, bali unampa nguvu msajili kufanya kazi ya wananchi ambayo ni kuhakikisha rasilimali zao zinatumika sawasawa.
Kesi ya kupinga muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa imefunguliwa na Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, Joram Bashange na Salim Biman wote wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa niaba ya muungano wa wanachama wa vyama 10 vya upinzani, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Hata hivyo Mahakama Kuu ya Tanzania imeamua shauri la kesi ya kupinga muswada wa vyama vya siasa isikilizwe kwa muda mfupi kwa kuwa kuna maslahi mapana ya umma, hivyo itasikilizwa Januari 11, 2019.