Alhamisi , 6th Jun , 2024

Wakati awamu ya tano ya zoezi la uchimbaji wa makaburi iliyoanza Jumatatu baada ya mapumziko ya miezi minane huko katika msitu wa Shakahola, miili mingine mitatu imefukuliwa na kuongeza wasiwasi kuwa bado kuna miili mingi zaidi iko ardhini.

Maafisa wa Ulinzi, Shakahola

Katika siku ya nne kumeshuhudiwa mabaki ya wahanga wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa mhubiri mwenye utata Paul Mackenzie yakiendelea kupatikana, huku maafisa wanaoshughulika na utaftaji huo wakikiri kutambua makaburi zaidi ya 50 ambayo bado hayajafukuliwa.

Hali hii imezua hofu miongoni mwa raia wa Kenya huku wanaharakati wa kutetea haki za kibinaadamu, wakielezea wasiwasi kuhusu maiti zaidi inayohifadhiwa kwenye kontena Malindi, ambayo bado haijatambuliwa na wanafamilia, wanataka matokeo ya DNA kutolewa na familia kupewa miili.

Kwa zaidi ya mwaka moja sasa tangu shughuli ya kufukuwa miili kuanza, eneo hilo bado limesalia kutelekezwa na chini ya ulinzi mkali kwani bado ni eneo la uhalifu huku jumla ya miili iliyoopolewa tangu mwaka jana kwa sasa ikifikia 446.

Kwa sasa Serikali imesitisha zoezi hilo hadi Jumanne wiki ijayo wakati huu ambao mshukiwa mkuu wa mauaji hayo Mhubiri Paul Makenzie akiendelea kushikiliwa na maafisa wa polisi, kwa kusababisha vifo vya waumini wake kutokana na itikadi za Dhehebu la Good News Intenational Kanisa ambalo alikuwa akiliongoza.