Moja ya shule zilizowahi kuungua kwa moto
Hayo yameelezwa bungeni leo Mei 11, 2021 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. George Simbachawene, wakati akijibu swali la Mheshimiwa Shally Josephat Raymond (Mbunge Wa Viti Maalum) ambalo lilihoji, Je, ni matukio mangapi ya moto yametokea kwenye Shule na masoko katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na Je, uchunguzi uliofanyika ulibaini vyanzo vya moto huo ulisababishwa na nini?
''Mheshimiwa Spika, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita kuanzia mwaka 2016 hadi 2020 lilipokea taarifa 175 za matukio ya moto kwenye Shule na taarifa 55 za matukio ya moto kwenye masoko,'' amesema.
Ameongeza kuwa, chunguzi mbalimbali za vyanzo vya matukio ya moto katika masoko na mashuleni, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilibaini vyanzo vya moto kuwa ni migogoro baina ya Wanafunzi na menejimmenti za Shule, matumizi ya umeme yasiyosahihi, uhalifu, uchomaji wa makusudi (hujuma), hitilafu za umeme, uchakavu wa mifumo ya umeme na uzembe kwa kuacha moto kwenye majiko ya mkaa.
Amesema ili kudhibiti matukio hayo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea na mikakati ya kuzuia majanga ya moto kwa kufanya ukaguzi wa majengo na kutoa ushauri na mapendekezo ya kitaalamu yakiambatana na utoaji wa elimu ya kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto na pia kusisitiza kuwepo kwa vifaa vya awali vya kuzima moto (fire extinguishers) na kung’amua moto (fire detectors) na uwepo wa Walinzi katika maeneo husika.