Jumapili , 3rd Jul , 2022

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba, ameziagiza idara na vitengo vya Wizara hiyo kuhakikisha zinatimiza wajibu wake kwa ufanisi ili kuyafikia matarajio makubwa ya wananchi kutokana na mambo ambayo Serikali imejipambanua kuyatekeleza kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Emmanuel Tutuba

Tutuba ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati wa Kikao kazi cha watumishi wa Wizara hiyo kilichoangazia tathmini ya kiutendaji katika kuwatumikia wananchi ambapo amesisitiza kuwa taasisi na Idara zote zinazokusanya mapato kujipanga vizuri kuhakikisha mapato yanakusanywa ili kutimiza lengo la kiasi cha shilingi trilioni 41.9 kilichopangwa kukusanywa na kutumika kwa mwaka fedha 2022/23.

"Idara zote zinazohusika na ukusanyaji wa mapato ya ndani zihakikishe kunakuwa na usimamizi mzuri ili kazi zifanyike kwa uadilifu na kuweka mifumo madhubuti ili kuhakikisha hakuna ufujaji wa mapato ili mapato yote yakusanywe kwa wakati bila kuleta kero kwa wananchi” amesema Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha.

Akitoa tathmini ya utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2021/22, Bw.  Tutuba amesema kuwa eneo la usimamizi wa mapato ya ndani limefanikiwa ambapo mpaka Juni mosi mapato ya jumla yamefikia takribani asilimia 96, mapato ya Mamlaka ya Mapato Tanzania asilimia 98 na mapato yasiyo ya kodi ya Msajili wa Hazina yamefika asilimia 102.

Aidha Tutuba ameeleza kuwa kwa mara ya kwanza Serikali imeweza kutoa fedha za miradi ya maendeleo kufikia asilimia 86, jambo ambalo halijawahi kufikiwa kwa takribani miaka 10.