Jumatatu , 22nd Sep , 2014

Jeshi la polisi nchini Tanzania limetakiwa kujiangalia upya katika utendaji wa kazi zake na kuacha kukiuka haki za binadamau ikiwemo kutowapiga ama kuwatisha waandishi wa habari wakati wanatekeleza majukumu yao ya kikazi.

Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Wananchi CUF Prof. Ibrahim Lipumba wakati alipokuwa akitoa msimamo wa chama hicho juu ya kupigwa hadi kujeruhiwa kwa waandishi wa habari tarehe 17 mwezi huu wakati walipokuwa wakitekeleza majukumu yao nje ya Jengo la Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.

Aidha Prof Lipumba amelalamikia kitendo cha jeshi la polisi kuzuia mikutano ya vyama vya upinzani ukiwemo mkutano wa CUF wa Bububu Zanzibar kwa madai kwamba bunge la katiba linaendelea.

Wakati huo huo, serikali ya Tanzania imesema iwapo mauaji ya watu wenye albino yataendelea kuwepo hapa nchini yanaweza kuhatarisha amani na usalama wa nchi hivyo ni lazima mauaji hayo yakomeshwe kwa nguzu zote.

Hayo yameelezwa jana jijini Dar es -Salaam na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii nchini Dkt. Seif Rashid wakati wa maadhimisho ya siku ya amani duniani yanayoadhimishwa kila mwaka ya Septemba 21.

Akiongea katika maadhimisho hayo mkurugenzo wa shirika la Under the same sun Vicky Mtetema amelalamikia kucheweshwa kwa kusikilizwa kesi za mauji ya watu wenye albinism.