Waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi Bwn. Sulemani Lukanga kwa tuhuma za kununua gari hewa la kubebea takataka kwa kiasi cha shilingi 92,750,000/= na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa skimu ya umwagiliaji ya Kakese kiasi cha shilingi miambili tisini na nne 294,000,000/= kinyume kabisa na sheria za utawala bora.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Eng. Boniface Nyambele anaetuhumiwa kwa uuzaji wa nyumba za serikali bila kufuata sheria za uuzwaji wa mali za umma.
Waziri wa Nchi ameagiza nafasi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma ikaimiwe na Mhandisi Sultan Imari Ndilowa ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maji, Manispaa ya Kigoma, nafasi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda ikaimiwe na Ndugu Lauteri John Kanoni ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Aidha Waziri amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote Nchini kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao wafuate Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote ambao watakiuka matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu na kutoweka mbele maslahi ya Umma.

