Jumatano , 13th Dec , 2017

Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Dk Mwigulu Nchemba amefanikiwa kumaliza mgogoro wa ardhi ambao umedumu kwa miaka zaidi ya tisa ambao ulifikia kuhatarisha amani ya kijiji cha Hurui jimbo la Kondoa vijijini wilaya ya kondoa mkoa wa Dodoma.

Mgogoro huo uliomalizwa Dk. Nchemba na umesababishwa na baadhi ya watu ambao si wajumbe wa kijiji kuuza eneo la kijiji la malisho mwaka 2009 bila mkutano wa kijiji kushirikishwa na kusababisha hali ya sitofahamu mpaka leo.

Imeelezwa kwamba jitihada za wananchi kutafuta haki ya eneo hilo kwa njia za kisheria hazikuzaa matunda kwani walishindwa katika kesi zote mbili walizofungua katika Mahakama ya Ardhi ya wilaya na mkoa, hali iliyopelekea Mbunge wa Kondoa Vijijini Dk. Ashatu Kijaji kumwita Waziri Nchemba kusaidia kutuliza taharuki hiyo.

Kwa upande wake Dk. Nchemba baada ya kusikiliza pande zote mbili za kijiji na serikali ya wilaya ameagiza eneo hilo liendelee kutumika kama lilivyopangwa tangu mwaka 1972 kuwa eneo la malisho, amewataka wananchi na viongozi wa vijiji waache kuuza maeneo kinyemela kwani ndio chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi katika vijiji nchini.

Naye Mbunge Kijaji amesema amechoka na migogoro ya ardhi katika jimbo lake yule ambaye atawafikisha katika migogoro watashughulika naye kwa sheria na taratibu za nchi.

Aidha Dk Ashatu amesema kuwa kwasasa hawawezi fanya shughuli za maendeleo katika baadhi ya vijiji kama kujenga madarasa na miundombinu ya maji na umeme kwasababu ya migogoro  ya ardhi iliyopo.