
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Majaliwa ameyasema hayo bungeni leo mjini Dodoma wakati akijibu maswali ya papo kwa papo kutoka kwa wabunge, ambapo Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Freeman Mbowe ameuliza swali kuhusu kupungua kwa mizigo bandarini na athari zake kwa uchumi.
“Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji ilikwenda bandarini na kubaini kuna upungufu wa mizigo hivyo serikali inataka ipate wadau gani wakati wadau wenyewe wanalalamika kuhusu mizigo yao , na watalii wamepungua hivyo serikali inataka ione nini ili ijue kwamba uchumi umeshuka? Ameuliza Mbowe.
Kuhusu suala la kupungua mizigo bandarini Waziri Mkuu amesema suala la mdororo kwa usafirishaji wa mizigo kwa njia ya meli umeshuka duniani kote kwa sababu ya kuporomoka kwa bei ya gesi na mafuta.
Amesema kuwa wiki moja iliyopita serikali imepata barua kutoka kwa wafanyabiashara wa DRC ikisema kwamba wataanza kupitisha mizigo yao kupitia bandari ya Dar es salaam, Rwanda nao wameihakikishia serikali kwamba mizigo yao pia itapitia Bandari ya Dar es Salaam hasa kwa mkakati wa pamoja wa ujenzi wa reli ya ‘Standard Gauge’ inayotoka Dar es Salaam, Tabora hadi bandari ya Isaka na kuunganishwa na reli hiyo hadi Rwanda.
Waziri Mkuu amesema serikali haijashindwa kuongoza nchi na kuwataka watanzania kuendelea kuiamini.
Amesema serikali ya awamu ya tano itaongoza nchi kwa mafanikio makubwa na katika sekta zote, kazi ambayo imeshaanza katika baadhi ya maeneo.
“Serikali hii haijashindwa kuongoza nchi hii nataka niwahakikishie wabunge na wananchi wote tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa sana kwenye sekta zote kazi hiyo imeanza katika maeneo ambayo tunadhani taifa hili litapata maeneleo makubwa.
Aidha Waziri Mkuu amesema suala la uchumi ni suala endelevu na serikalI inaendelea kulifanyia kazi kubwa ya kufanya kampeni ya kupata wafanyabiashara wengi zaidi ili kuimarisha uchumi.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha inaendelea kuimarisha amani na ulinzi kwenye maeneo yote nchini na kwamba vyombo vya dola viko macho. “Watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji watakamatwa popote walipo na kuchukuliwa hatua za kisheria,; amesema.
Amesema hatua hiyo inatokana na matukio ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni ambapo raia wasiokuwa na hatia na askari waliuawa katika maeneo ya Vikindu mkoani Pwani, Tanga na Mwanza. Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani
Katika swali lake, Bw. Ngonyani alitaka kujua ya Serikali kuhusu kukomesha mauaji hayo, yanayotokea kwa watu wasio na hatia pamoja na askari, ambapo Waziri Mkuu, alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa wananchi na familia, ambazo ndugu zao walipoteza maisha katika mauaji hayo.