Jumanne , 27th Jul , 2021

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amesema serikali haijamlazimisha na wala haitamlazimisha mwananchi kuchanjwa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO-19, hivyo amewataka Watanzania wapuuze upotoshaji unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii. 

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ruangwa kwenye mkutano wa hadhara ambapo amewasisitiza watanzania kujikinga na UVIKO-19 kwa kuendelea na tabia ya kunawa mikono mara kwa mara na maji safi yanayotiririka, watumie vitakasa mikono pamoja na kuvaa barakoa zilizothibitishwa na mamlaka husika
 

"Hakuna aliyelazimishwa kuchanja chanjo hiyo na wala hakuna mahali palipoandikwa kwamba lazima wananchi wachanjwe, chanjo ni hiyari tusipotoshane kwa sababu hakuna Serikali inayoweza kuandaa mpango wa kuwaangamiza wananchi wake," amesema Majaliwa.
 
Pia Mhe. Majaliwa amesema Serikali imeleta chanjo hiyo ili kutoa fursa kwa Watanzania watakaohitaji kuchanjwa kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 waweze kuipata kwa ukaribu na urahisi zaidi na si vinginevyo. 
  
Aidha, Waziri Mkuu amesema ni vema kwa sasa wananchi wakajiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima nakuwataka wananchi wafanye mazoezi ya mara kwa mara kulingana na afya zao pamoja na mazingira yanayowazunguka na wazingatie lishe bora.