Jumatatu , 19th Feb , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi Bw. Alphonce Sebukoto na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.

Waziri Majaliwa amechukua hatua hiyo baada Mwanasheria huyo kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya sh. milioni 279.

Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Bw. Sebukoto wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

“Mwanasheria utasimama kazi kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo husika na uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. Hatuta kuonea lakini hatuwezi kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya”, amesema Majaliwa.

Aidha, Waziri Majaliwa amesema mwanasheria huyo Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya ukurugenzi aliidhinisha malipo ya sh.milioni 279 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Anthony Bahebe.

“Mwanasheria amemlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri baada ya kuifikisha Halmashauri yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati kazi yenyewe ilikuwa haijaisha na aliharakisha malipo hayo kipindi ambacho Mkurugenzi hayupo”, amesisitiza Majaliwa.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao. Amesema fedha alizolipwa Bw. Bahebe zingeweza kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.