Jumanne , 3rd Oct , 2023

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandya awasimamishe kazi watumishi wawili wa jiji hilo huku akiagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa huo arudishwe wizarani na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ameagiza ujenzi wa ghorofa uliositishwa na Mkuu wa mkoa huo Amos Makalla uendelee kwenye viwanja namba 194 & 195 kitalu ‘U’ Rwagasore, jijini Mwanza na wamiliki wa viwanja hivyo wakabidhiwe hati zao kama alivyokuwa ameelekeza awali.

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Oktoba 3, 2023, kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma cha viongozi wa majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Tanga na Dodoma ili kujadili migogoro ya ardhi iliyokithiri kwenye majiji hayo.

"Ninaagiza Katibu Tawala wa Mkoa wasimamishe kazi Mkuu wa Idara ya MipangoMiji, Robert Phares na Afisa Mteule na Mkuu wa Kitengo cha Ardhi katika Jiji la Mwanza Halima Iddi Nasoro. Na Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi (Mwanza) Elia Kamihanda arudishwe makao makuu na achukuliwe hatua za kinidhamu," ameagiza Waziri Mkuu

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wawafuatilie na kuwarejesha Dodoma watumishi 11 waliokuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili wajibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha, kupora maeneo ya wananchi na kugawa maeneo ya wazi.

"Watumishi wa Jiji la Dodoma ni Josephat Mafuru (aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji), Scorpion Philip, Lennis Ngole, Allen Mwakanjuki, Aisha Masanja, Agusta Primo, Azory William Byakanwa, Frezia Kazimoto, Premin Nzenga, Stella Komba na Thabiti Mbiyagi. Hawa ni wachache miongoni mwa wengi waliohusika kusababisha migogoro, watafutwe na waje kujibu tuhuma dhidi yao," amesema.