Jumanne , 8th Nov , 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiomba Serikali ya Uingereza ihamasishe wawekezaji zaidi kutoka nchini humo ili waje kuwekeza kwenye sekta ya viwanda.

Sarah Cooke - Balozi wa Uingereza nchini

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza hapa nchini, Bibi Sarah Cooke alipokutana naye ofisini kwake Bungeni, mjini Dodoma.

“Mheshimiwa Balozi utusaidie kualika wawekezaji wengi zaidi kwenye maeneo ya kilimo, viwanda vya usindikaji mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji, sekta ya mafuta na gesi, nishati na ujenzi wa makazi hasa kwa mkoa wa Dodoma ambako hivi sasa ni Makao Makuu ya Serikali,” amesema.

Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa

Amemweleza Balozi huyo kwamba Tanzania imedhamiria kuwa nchi ya uchumi wa kati na hivyo imejipanga kuwa na viwanda vya kutosha ili iweze kusindika mazao yake hapa nchini na itoe ajira kwa wananchi wake.

Kwa upande wake, Balozi Cooke ambaye alifika kujitambulisha rasmi, amesema ameguswa na juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukabiliana na masuala ya ufisadi na rushwa. “Kaulimbiu yenu kwamba rushwa haikubaliki (zero tolerance on corruption) inaonesha jinsi mlivyodhamiria kupambana na baa hili,” amesema.

Amesema Uingereza inaongoza miongoni mwa nchi zenye wawekezaji wengi hapa nchini na kwamba inaendeleza mpango wake wa uwekezaji ambao unalenga maeneo makuu manne ambayo ni gesi na mafuta; kilimo; nishati jadidifu na uimarishwaji wa mazingira ya kufanya biashara.