Jumatano , 6th Dec , 2017

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu ) Mhe. Jenista Mhagama ameitaka (MIVARF) kuongeza thamani ya biashara za mifugo wilayani Longido.

Waziri Mhagama ametoa agizo hilo baada ya kukagua soko la kimkakati lililojengwa na serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Program ya miundombinu ya masoko, uongezaji thamani na huduma za kifedha vijijini (MIVARF).

Soko hilo lililopo wilayani Longido litawanufainisha wananchi wapatao 142,000 wa wilayani humo ambao asilimia 95 ni wafugaji na huzalisha bidhaa zitokanazo na mifugo.

Soko hilo la kimkakati limeingiza mapato ya jumla ya kiasi cha shilingi milioni 106 kwa mwaka 2016/17, na kusaidia wilaya hiyo kuweka rekodi ya kuingiza mapato ya bilioni 1.3 kwa mwaka kitu ambacho hakikuwahi kutokekea hapo awali.

MIVARF ni Programu ya Miundombinu ya Masoko na Huduma za kifedha vijijini, iliyobuniwa mwaka 2011 na serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) na inatekelezwa katika mikoa 29 nchini.